Chupuchupu! Mwanadada anayeng’ara kunako tasnia ya filamu za Kibongo,
Jacqueline Wolper, juzikati almanusra apigwe risasi kwenye kituo kimoja
cha mafuta kilichopo Tegeta (jina linahifadhiwa) jijini Dar es Salaam,
baada ya kuibuka kwa timbwili zito eneo hilo, Risasi Mchanganyiko
linakupa mkasa mzima.
Tukio hilo la aina yake, lilijiri mishale ya saa tano usiku wa Juni
12, mwaka huu ambapo kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika, Wolper
alinusurika kupigwa risasi na mlinzi wa kituo hicho cha mafuta baada ya
kutokea hali ya sintofahamu kati yake na mfanyakazi mmoja kwenye kituo
hicho.
“Ishu yenyewe ni kwamba, kuna muda Wolper alifika pale sheli (Sheli
ni neno lililozoeleka likimaanisha kituo cha mafuta, lakini ukweli ni
kuwa jina hilo ni la kampuni ya mafuta yenye makao makuu yake Nchini
Marekani) akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Mark X, lile linalodaiwa
kuwa ni la mpenzi wake wa sasa, Harmonize (Rajab Abdulkan).
“Akaongeza mafuta na kuondoka zake, dakika kadhaa baadaye,
tulishangaa kumuona Wolper akirudi tena na kwenda mpaka kwa yule dada
aliyemuuzia mafuta lakini safari hii alionekana kuja kwa shari.
“Akashuka kwenye gari na kuanza kumuwakia yule dada kwa madai kwamba
amemuibia mafuta na kusababisha gari lake limzimikie njiani wakati
alitoa shilingi elfu ishirini,” kilisema chanzo chetu.
Kwa mujibu wa chanzo, timbwili la aina yake lilizuka eneo hilo baada
ya msichana huyo kuanza kumjibu mbovu msanii huyo ambaye hakukubali,
Wolper akakinukisha kwa kumvaa na kuanza kumshushia kichapo, tukio
lililokusanya umati wa watu.
Ilibidi mlinzi wa kituo hicho cha mafuta, aingilie ugomvi huo. Hata
hivyo, mlinzi huyo alionekana kumtetea zaidi mfanyakazi mwenzake na
kumkandamiza Wolper, jambo lililozidi kumpa hasira msanii huyo.
“Alipoona wanasaidiana, Wolper aliwachenjia wote wawili, jambo
lililosababisha mlinzi huyo aondoke eneo hilo lakini aliporejea, alikuwa
na bunduki yake ya lindo mkononi, akaikoki na kutaka kumpiga risasi
Wolper,” kilisema chanzo chetu na kuongeza kuwa kuona hivyo, Wolper
alikimbilia ndani ya gari lake na kutoka nduki, akiacha watu wengi
wakiwa wamekusanyika kituoni hapo.
Baada ya kusikia maelezo hayo kutoka kwa chanzo chetu, Risasi
Mchanganyiko lilimtafuta Wolper ambaye baada ya kusomewa mashtaka hayo,
alikiri kutokea kwa tukio hilo.
“Dah, ni kweli nilikutana na matatizo hayo usiku, ambapo nilikuwa
naenda Tegeta baada ya kufika njiapanda flani pale, gari lilipungua
mafuta nikaingia kituoni na kuongeza ya elfu 20, wakati naongeza
nilihisi kabisa yule dada ananiibia lakini sikumjali, nikalipa na
kuondoka.
Nilipofika mbele kidogo tu gari lilizima,” alisema Wolper na
kuongeza: “Ilibidi nifanye utaratibu wa kupata mafuta mengine kisha
nikageuza na kurudi mpaka pale sheli kwa lengo la kudai haki yangu ndiyo
kukatokea timbwili hilo kwani mlinzi wa pale alikuwa anamsaidia yule
dada aliyeniibia.”
“Wakati nikiwa najihami maana yule mlinzi alikuwa akinikaba,
nilimpiga kibao, akakimbilia bunduki yake na kuanza kuikoki akitaka
kunipiga risasi.
“Baada ya kuona amefikia hatua hiyo niliingia haraka kwenye gari
langu na kuondoka zangu kwani nilihisi walikuwa na njama moja ya
kuniibia mafuta na walipoona nimerudi kulalamika ndiyo wakaamua
kunifanyia vurugu, kweli sikufurahishwa na tabia yao kwanza ni wezi
wakubwa wa mafuta hao,” alisema Wolper.
No comments:
Post a Comment